Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
USHINDANI wa kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umefikia hatua mpya
baada ya CCM kuibuka na mkakati wa kumtumia Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Kabwe, kupambana na CHADEMA waziwazi.
Katika mkakati huo CCM imepanga kukodisha helikopta ya kumpeleka
Zitto katika mikoa minne kwa gharama ya sh milioni 50 mara tu baada ya
CHADEMA kuhitimisha Operesheni yao ya M4C Pamoja Daima.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vilivyo karibu na Zitto na CCM,
yeye na chama hicho sasa wana adui mmoja – CHADEMA; na wameamua kujibu
mapigo baada ya kuridhika kwamba kwa vyovyote Zitto amekwisha kupoteza
uanachama wake katika CHADEMA.
Nia yao ni kumtumia Zitto kuleta mpasuko katika CHADEMA, na kufunika
mjadala wa mgogoro wa CCM, kero za wananchi na mchakato wa Katiba mpya.
Zitto ambaye alivuliwa nyadhifa zake zote ndani ya CHADEMA – Naibu
Katibu Mkuu Bara, Mjumbe wa Kamati Kuu, Mjumbe wa Baraza Kuu na Naibu
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni – anatarajia kutumia
helikopta yenye uwezo wa kubeba watu wanne, ambayo inadaiwa kukodishwa
na wapinzani wa CHADEMA.
Kwa mujibu wa habari hizo, lengo la ziara ya Zitto ni kujibu mapigo
ya CHADEMA, hasa katika maeneo ambayo baadhi ya makada na viongozi wa
chama hicho wamepita na kuzungumzia hatima yake kisiasa, hasa walipojibu
maswali ya wananchi kuhusu sakata lake kuvuliwa uongozi kwa tuhuma za
usaliti, na hatimaye Zitto kwenda mahakamani kuzuia chama kujadili
uanachama wake.
Katika kesi ya msingi, Zitto aliyewahi kuwa maarufu
akiwa kiongozi wa CHADEMA, anaomba arudishiwe nyadhifa zake zote, na
apatiwe nakala za uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ili aweze kukata rufaa
Baraza Kuu.
Taarifa zinasema tayari chama kimempatia nyaraka hizo, lakini kwa
mujibu wa Katiba ya CHADEMA, Zitto amekwisha kujiondoa kwenye chama
hicho kwa kupeleka shauri mahakamani.
Taarifa za Zitto kuanza ziara mikoani zilianza kusikika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mikoa
iliyotajwa ni Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Morogoro na Dar es Salaam,
ingawa maandalizi yanaendelea na kuna uwezekano wa kubadili baadhi ya
mikoa kulingana na mkakati wao.
Kwa hadhi yake ya sasa, CHADEMA
imeshasema haitahusika na mikutano yake, na wanachama wake
hawatajihusisha nayo. Uratibu wa mikutano yake unafanywa na viongozi
waandamizi wa CCM.
Baadhi yao walizungumza na gazeti hili kwa
kujitapa kwamba hii ndiyo njia ya kuimaliza CHADEMA, lakini hawakutaka
kutajwa majina gazetini.
Iwapo Zitto atakubali ufadhili huo wa
CCM na kuendelea na mikutano yake, ni wazi atakuwa amekamilisha ushahidi
wa kinachodaiwa na chama chake kwamba amekuwa akikisaliti kwa masilahi
ya CCM.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa CCM walipoombwa maelezo
juu ya urafiki wao na Zitto kiasi cha kumkosanisha na chama kilichomlea
kisiasa, CHADEMA, walisema kwamba urafiki uliopo si wa Zitto na CCM,
bali Zitto na Rais Jakaya Kikwete.
Gazeti hili linafahamu kwamba
wakati fulani mwaka juzi Zitto alipobanwa na wabunge wenzake kuhusu
tabia zake za kuwasaliti kwa Rais Kikwete, alisisitiza kuwa Rais Kikwete
ni rafiki yake binafsi, kwa hiyo wamwelewe.
Vilevile, wapo
wanaohoji nia ya ziara hii wakati kwa muda mrefu amekuwa akikwepa
kuambatana na viongozi wenzake katika ziara na operesheni nyingi za
kichama.
Wanasema kwa kuwa operesheni ya sasa ya CHADEMA imepewa
jina la M4C Pamoja Daima, kitendo cha CCM kuandaa ziara ya Zitto na
kumkodishia helikopta, ni uthibitisho kuwa Zitto hayuko pamoja na
CHADEMA tena.
Wameongeza pia kuwa kama hilo litafanyika, litakuwa
limemwingiza Zitto katika orodha ya makada kadhaa wa upinzani
waliotumikia CCM baada ya kufukuzwa au kunyimwa fursa za uongozi katika
CHADEMA, kama Tambwe Hiza, Dk. Aman Walid Kabourou na Dk. Masumbuko
Lamwai.
Alipotafutwa athibitishe kuhusu ziara hii na kama ni kweli inafadhiliwa na CCM, Zitto hakuweza kupatikana.
Mbowe kuwania tena uenyekiti
Katika
hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa kamwe hatakiacha chama hicho
katika uchanga wa harakati za kulikomboa taifa kama kiongozi wake wa
juu.
Akihutubia katika mikutano ya Operesheni M4C Pamoja Daima
katika sehemu mbalimbali mkoani Morogoro jana, mwenyekiti huyo
alisisitiza kuwa, bado atagombea nafasi ya uenyekiti kwa lengo la
kuendeleza harakati za ukombozi wa pili wa taifa hili.
Bila
kutaja jina, Mbowe alionya kuwa wenye fikra za kuachiwa chama hicho
kikiwa katikati ya ukombozi huo hawatapata nafasi, kwa sababu hawana nia
thabiti ya kukiendeleza, bali wana nia ya kukibomoa kwa kutumiwa na
wapinzani wa CHADEMA.
“Makamanda, kumbukeni kuwa chama hiki na
sisi viongozi wake tumepita katika majaribu makubwa na hata kukoswakoswa
kuuawa. Mimi nimekoswakoswa kuuawa kwa bomu huko Arusha, lakini pia
kuna watu wamepoteza maisha, wamefungwa jela, wengine wamekuwa vilema,
halafu watu wengine wanatusaliti kwa kupewa visenti ili wakivuruge chama
na wanataka tuwape chama. Huu ni uendawazimu,” alisema.
Mwenyekiti
huyo alisema CCM imekuwa ikifanya jitihada za kuihujumu CHADEMA kwa
mbinu mbalimbali, zikiwemo za kupandikiza migogoro, jambo ambalo
limeshindwa kufanikiwa kwani Mungu ameweka mkono wake ili
kisisambaratike.
“Harakati hizi tunazofanya za kuwakomboa
Watanzania mjue tunahatarisha maisha yetu, tumejaribiwa kushawishiwa
ndani na nje ya Bunge ili tuwe kondoo, tumekataa. CCM wamekuja na mbinu
za kupandikiza migogoro wameshindwa na sasa wanaomba nife wakifikiri
nikifa na CHADEMA itakufa. Nawaambia CHADEMA haifi kwa kuwa tumezalisha
makamanda wengi, watakiendeleza,” aliongeza Mbowe.
Akielezea kwa
mara ya kwanza kwa undani zaidi kuhusu mauaji ya Arusha, mwenyekiti huyo
alisema wana ushahidi wa kutosha kwamba polisi walihusika na mauaji
hayo na kuongeza kuwa waliohusika ni polisi wa kutoka mkoani Morogoro.
“Kwa
mara ya kwanza niliseme hili, mauaji ya Arusha yaliyofanyika kwa
kurusha bomu katika mkutano wa kampeni za CHADEMA, yalifanywa na polisi
ambao walitoka mkoani Morogoro. Ndiyo maana tunaendelea kumwambia Rais
Jakaya Kikwete aunde tume ya kimahakama ili kupata ukweli wa jambo
hili,” alisema.
Kuhusu Katiba
Akizungumzia
msimamo wa CHADEMA kuhusu muungano, Mbowe alisema chama hicho kinaunga
mkono maoni yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa
na Jaji Joseph Warioba, ya serikali tatu.
Alisema hata tafiti
mbalimbali zilizofanyika, zikiwemo za wanasheria na wachumi zinaonyesha
kuwa Muungano utaimalika zaidi chini ya muundo wa serikali tatu.
“Nawaonya
Wana CCM wasijaribu kuingilia mjadala wa Bunge la Katiba na kama
wanataka nchi ichimbike, basi walazimishe serikali mbili,” alisema
Mbowe.
“Zipo tetesi za CCM kutaka kupitisha hoja zao kwa nguvu
kutokana na idadi yao ndani ya wabunge zaidi ya 600, wakiwemo 356 wa
Bunge la Tanzania Bara, 84 kutoka Zanzibar na 201 kutoka makundi
mbalimbali watakaokwenda kwenye bunge hilo. Wasidanganyike kwamba
wanaweza kutumia wingi wao kubadilisha maoni ya Watanzania kuhusu
serikali tatu,” alisisitiza Mbowe.
Halima Mdee anguruma
Naye
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, ambaye yuko katika msafara wa mwenyekiti
huyo, alisema vijana wengi wanaochipukia katika siasa kupitia chama
hicho, wamelelewa na Mbowe, ambao leo wamekuwa chachu ya mabadiliko
nchini.
“Ukweli ni kwamba kamanda huyu wa anga (Mbowe), ndiye
ametulea vijana wengi nikiwemo mimi, tena wengine hatukuwa na ujasiri
tulionao sasa, asiwadanganye mtu, hasa sisi vijana kwamba tuliingia
CHADEMA na umaarufu, hawapo hao, tumelelewa na huyo kamanda,”
alisisitiza huku akipigiwa makofi.
CHANZO NI TANZANIA DAIMA
Tafadhali bofya like kama bado hujabofya kwenye page yetu