Wednesday, January 29, 2014

Matokeo ya Vodacom premier League ya leo haya hapa:Yanga washushwa kileleni.


MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC wameshushwa kileleni mwa ligi hiyo leo kufuatia kulazimishwa sare ya bila kufungana na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. 
Matokeo hayo yanaifanya Yanga itimize pointi 32 baada ya kucheza mechi 15 na kuipisha Azam FC kileleni, ambayo imetimiza pointi 33 baada ya kuifunga Rhino Rangers bao 1-0 leo.   Mchezo ulisimama mara mbili kwa dakika moja na ushei ili kupisha zoezi la uokotaji wa chupa za maji zilizojazwa mikojo na tupu zilizorushwa uwanjani na mashabiki wa timu hizo.
Kwanza ilikuwa dakika ya 29, mashabiki wa Yanga waliporusha chupa baada ya kukerwa na kitendo cha mshika kibendera nambari moja kumezea kitendo cha beki wa Coastal Union Juma Nyosso kuunawa mpira uliopigwa na Didier Kavumbangu katika eneo la hatari.

Dakika tisa baadaye, mashabiki wa Coastal nao walirusha chupa langoni mwa Yanga kufutia timu yao kushambuliwa na Wana Jangwani. 

Yanga SC ilitawala mchezo kipindi cha kwanza na Coastal walitawala kipindi cha pili.
Huo unakuwa mchezo wa nne Yanga SC kucheza chini ya kocha wake mpya, Mholanzi Hans van der Pluijm ikishinda mechi mmoja tu.

Awali Mholanzi huyo aliyefukuzwa fukuzwa timu kibao Ghana na St George ya Ethiopia kwa matokeo mabaya kabla ya kutua Jangwani, alitoa sare mbili katika ziara ya Uturuki na akashinda dhidi ya Ashanti United kwa taabu 2-1 Jumamosi katika Ligi Kuu.

Katika mchezo wa leo uliotawaliwa na vurugu za mashabiki, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbangu, Mrisho Ngassa/Nizar Khalfan dk83 na David Luhende/Jerry Tegete dk66.

Coastal Union; Shaaban Kado, Hamad Juma, Abdi Banda, Juma Nyosso, Mbwana Bakari, Jerry Santo, David Lyanga, Crispian Odula, Lutimba Yayo/Mohammed Miraj dk88, Haruna Moshi na Kenneth Masumbuko/Mohamed Soud dk78.


Mbeya City 1-1 Ruvu Shooting
 Nayo Mbeya City ilipunguzwa kasi na Ruvu Shooting baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye uwanja wa Mabatini, Mlandizi ikiwa ni pointi ya kwanza kwa kocha Tom Olaba tangu aanze kuinoa Ruvu.
Ruvu walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Jerome Lembeni kabla ya Jeremia John kusawazisha. Mabao yote yakifungwa katika dakika 15 za awali za kipindi cha kwanza.


AZAM FC 1-0 Rhino Rangers
  AZAM FC imepanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia ushindi wa bao 1-0 jioni hii dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Bao pekee la Azam limefungwa na mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche dakika ya 26 kwa shuti kali baada ya kuukuta mpira uliozuiwa na mabeki wa Rhino, kufuatia shuti la ndugu yake kutoka nchi moja, Ismael Kone.

Azam sasa inafikisha pointi 33 na kupanda kileleni, ikiiteremsha Yanga iliyolazimishwa sare ya bila kufungana na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga leo ambyo sasa inakuwa na pointi 32.    

Tafadhali bofya like kama bado hujabofya kwenye page yetu

Share this article

0 comments:

ASANTE KWA KUTEMBEA BLOGU YAKO::KARIBU SANA

Toa Mani yako Hapa usiogope Tuko Pamoja

Post a Comment

 
Copyright © 2014 Chopa News • All Rights Reserved.
| Template Design by Anga Zio Team • Powered by Blogger online
back to top