Saturday, December 27, 2014

MTOTO ASOMBWA NA MAJI NA KUFARIKI.

MTOTO wa miaka sita, Bernard Benjamin ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nyamunge, wilayani Ilemela jijini Mwanza, amesombwa na mafuriko na mwili wake kukaa siku kumi na tano bila kuharibika.

Mafuriko yaliyosababisha kifo cha marehemu mtoto Bernard Benjamin.

Tukio hilo lilijiri Desemba 2, mwaka huu kwenye Mto Kenge jijini hapa, maeneo ya Mabatini, Wilaya ya Nyamagana baada ya kujaa maji ambapo marehemu alisombwa na mafuriko hadi pembezoni mwa Ziwa Victoria.

Baba mzazi wa marehemu Bernard, Benjamin David alisema siku ya tukio yeye alikuwa safari na mama wa mtoto alikuwa kazini, watoto walibaki na msichana wa kazi nyumbani.

Baba wa marehemu Bernard Benjamin akihuzunika.

“Ilikuwa Jumanne asubuhi, mvua kubwa sana ilinyesha kwa saa moja na nusu hivi na kusababisha mafuriko. Watoto wangu wote walikuwa nyumbani, lakini mvua ilipokatika walitoka nje na kuanza kucheza.

“Marehemu alikuwa anaondoka bila kuaga kama mara tatu na kila alipofuatwa alikutwa akicheza pembezoni mwa mto huo ambao  umepita jirani na nyumba yangu.“Katika hali ya kushangaza mara ya tatu wenzake walimfuata na kuanza kurudi naye wakati huo marehemu alikuwa yupo nyuma ndipo aliteleza na kutumbukia kwenye maji ya mto.

Mwili wa marehemu Bernard Benjamin ukiwekwa kaburini.

“Alipiga kelele na wenzake walivyosikia sauti nao walipiga mayowe, mmoja wao alijitosa kwenye maji ili amuokoe lakini kasi ya maji ilimshinda na kujikuta akijiokoa mwenyewe kwa kushika mti, watu wakamuwahi na kumuokoa.

“Tuliutafuta mwili tangu siku hiyo hadi Jumatano ya Desemba 17. Saa 10 jioni mke wangu alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni muumini wa kanisa kwetu, akasema kuna mwili wa mtoto umekutwa ufukweni mwa Ziwa Victoria eneo la Miti Mirefu.

Mama mzazi wa marehemu Bernard Benjamin akiweka mchanga kaburini.

“Nilikwenda na kukuta polisi wameshafika. Nilipouona mwili niliutambua kuwa ni wa mwanangu akiwa ameshafariki dunia lakini haukuwa umeharibika.“Bado alikuwa na nguo alizovaa siku ya tukio, viungo vyake vyote vilikuwa salama ila mwili ulikuwa mweupe sana kutokana na kukaa muda mrefu kwenye maji.

Mtoto Bernard Benjamin enzi za uhai wake.

“Tuliupeleka mwili Hospitali ya Rufaa ya Bugando, madaktari walimfanyia uchungzi na kusema mwili haukuharibika kutokana na kufukiwa na mchanga mwingi kwenye maji, nilimshukuru Mungu kwa hilo,” alisema baba wa marehemu.Mazishi ya mtoto huyo yalifanyika Alhamisi ya Desemba 18, mwaka huu katika Makaburi ya Nyakato Sokoni jijini Mwanza.

BREAKING NEWS: Mtu mmoja afariki dunia baada ya kulipuliwa na bomu aliotaka kuwarushia askari polisi.



UNGANA NAMI KATIKA FACEBOOK KWA KUBOFYA Like HAPO JUU

Share this article

0 comments:

ASANTE KWA KUTEMBEA BLOGU YAKO::KARIBU SANA

Toa Mani yako Hapa usiogope Tuko Pamoja

Post a Comment

 
Copyright © 2014 Chopa News • All Rights Reserved.
| Template Design by Anga Zio Team • Powered by Blogger online
back to top