Friday, May 30, 2014

Majibu ya Zitto Kabwe juu ya madai ya kambi ya upinzani kuhusu Lekadutigite na Gombe Advisors haya hapa.

Kwenye Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ya Wizara ya Habari,Utamaduni na Michezo aliyoiwasilisha Bungeni leo hii muda mfupi uliopita. Waziri Kivuli Joseph Mbilinyi  ‘Sugu’ alimtaja Zitto Z. Kabwe kama Mmiliki wa Kampuni ya Leka Dutigite aliyofanya biashara isivyo halali na Mashirika ya Umma ya NSSF na TANAPA.

Hivi ndivyo ilivyokuwa sehemu ya hotuba hiyo.

Mheshimiwa Spika, Tarehe 13 Agosti, 2012, Msajili Msaidizi wa Makampuni katika Wakala wa Usajili wa Makampuni na Leseni (BRELA) alitoa Hati ya Usajili (Certificate iof Incorporation) kwa kampuni inayoitwa Leka Dutigite Limited. Kwa mujibu wa nyaraka za BRELA, Leka Dutigite Ltd. ina ofisi zake katika ghorofa ya kwanza ya jengo la City House lililoko katika Mtaa wa Mkwepu, Dar es SalaaM.

Mheshimiwa Spika,Katiba yaani Memorandum and Articles of Association, ya kampuni ya Leka Dutigite Ltd. iliyosajiliwa BRELA tarehe 13 Agosti, 2012 inaonyesha kwamba mwenye hisa nyingi katika kampuni hiyo ni kampuni nyingine inayoitwa Gombe Advisors Ltd. ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa za kibenki ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu imezipata, mnamo tarehe 10 Desemba, 2012, Hifadhi ya Taifa ya Saadani ilihamisha jumla ya shilingi 12,200,000 kwenda kwenye akaunti na. 0150357447800 iliyoko CRDB Bank tawi la Pugu Road, Dar es Salaam, inayomilikiwa na Leka Dutigite Ltd. Hifadhi ya Taifa ya Saadani inamilikiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), ambayo ni shirika la umma. Siku moja baadae, fedha hizo zilitolewa kwa pesa taslimu kutoka kwenye akaunti hiyo.

Baada ya hapo, kati ya tarehe 14 Januari na 7 Februari, 2013, akaunti ya Leka Dutigite Ltd. iliingiziwa jumla ya shilingi 28,600,000. Fedha hizi zote ziliingizwa kama fedha taslimu na mtu aitwaye Mchange (shilingi 3,600,000 tarehe 14 Januari, 2013) na Leka Dutigite (shilingi 25,000,000 tarehe 23 Januari na 7 Februari, 2013). Kufikia tarehe 7 Februari, 2013, fedha hizo zote zilikwishatolewa benki.

Mheshimiwa Spika, Tarehe 28 Februari, 2013, akaunti ya Leka Dutigite Ltd. iliingiziwa shilingi 32,367,000 na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Kwa mujibu wa taarifa za kibenki, siku hiyo hiyo, fedha hizo zilitolewa kwenye akaunti hiyo. Siku nne baadae, yaani tarehe 4 Machi, 2013, NSSF ilifanya malipo mengine kwenye akaunti ya Leka Dutigite Ltd., kwa mikupuo miwili, ya jumla ya shilingi 46,663,000. Siku hiyo hiyo, fedha hizo nazo zilitolewa kutoka kwenye akaunti hiyo kwa mikupuo miwili. Kwa hiyo, katika kipindi cha miezi mitatu katika ya tarehe 10 Desemba, 2012 na 4 Machi, 2013, Leka Dutigite Ltd. ililipwa shilingi 119,930,000 kwa utaratibu huo huo wa ingiza na toa fasta. Kati ya fedha hizo, shilingi 12,200,000 zililipwa na TANAPA na shilingi 79,027,000 zililipwa na NSSF.

Mheshimiwa Spika, Katika mazingira ya kawaida, sio kitu cha ajabu kwa mashirika ya umma kama NSSF na TANAPA kufanya biashara na watu au taasisi mbali mbali kama makampuni binafsi. Ukweli ni kwamba, kwa upande wa malipo yaliyofanywa na TANAPA, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu imeweza kupata nakala ya mkataba unaohusu Maandalizi ya Filamu (Documentary) kwa Ajili ya Kuhamasisha Shughuli za Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa Kutumia Wasanii Kutoka Kigoma. Mkataba huo umesainiwa tarehe 5 Desemba, 2012, kati ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Leka Dutigite Ltd. na una thamani ya shilingi 12,200,000, kiasi kile kile kilicholipwa na Hifadhi hiyo.

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, mazingira ya malipo haya sio ya kawaida. Hii ni kwa sababu ya uwepo wa kampuni ya Gombe Advisors Ltd. Kwa mujibu wa nyaraka za BRELA, kampuni hii ilisajiliwa tarehe 24 Novemba, 2011. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, ofisi za Gombe Advisors Ltd. ziko kwenye jengo la City House, Mtaa wa Mkwepu, Dar es Salaam, ziliko ofisi za Leka Dutigite Ltd. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, wakurugenzi wa Gombe Advisors Ltd. ni Zitto Zuberi Kabwe ambaye kazi yake inatajwa kuwa ‘mchumi’, na Raphael Ongangi ambaye anatajwa kuwa ‘mchambuzi wa fedha na vitega uchumi’ (Financial and Investment Analyst). Bwana Ongangi aliwahi kutajwa na gazeti la kila wiki la —– la tarehe 26 Desemba 2013 kuwa ni mmoja wa washauri wa Zitto Zuberi Kabwe na anasemekana kuwa msaidizi wake.

Mheshimiwa Spika, Zitto Zuberi Kabwe sio ‘mchumi’ anayetajwa katika nyaraka za BRELA zinazoihusu kampuni ya Gombe Advisors Ltd. pekee, bali pia ni Mbunge, tangu mwaka 2005, wa Bunge lako tukufu. Kama Mbunge, Mheshimiwa Zitto Kabwe ni ‘kiongozi wa umma’ kwa mujibu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, 1995. Sheria hii inawalazimu viongozi wa umma, wanapokuwa madarakani, kuwa “waadilifu, wenye huruma, utulivu, umakini na watakaoendeleza viwango vya juu vya maadili ili kujenga na kuendeleza imani ya umma kwa uadilifu wa Serikali.”

Aidha, viongozi wa umma “… watawajibika kutekeleza wajibu wao kwa umma na kuendesha shughuli zao binafsi kwa namna ambayo itaonekana na kuthibitika kuwa ni wazi kwa umma na haitatosheleza kwao kutekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria tu.” Vile vile, kuhusiana na maslahi binafsi, Sheria hii inaelekeza kwamba “… viongozi wa umma hawatakuwa na maslahi binafsi ambayo yanaweza kuathiriwa na maamuzi ya serikali wanayoshiriki katika kuyafanya.

Mwisho,kuhusiana na maslahi ya umma, viongozi wa umma wanatakiwa, pale wanapochaguliwa au kuteuliwa, kupanga masuala yao “kwa namna itakayozuia migongano ya maslahi ya wazi, iliyojificha au inayoonekana kuwepo na pale ambapo migongano hiyo inatokea kati ya maslahi binafsi na maslahi ya umma basi itatatuliwa kwa kuangalia zaidi maslahi ya umma.” Kwa kadri ya ufahamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, Mheshimiwa Zitto Kabwe hajawahi kutangaza maslahi aliyonayo kwenye mikataba ya Gombe Advisors Ltd. na Leka Dutigite Ltd. na NSSF na TANAPA.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe sio tu ni Mbunge anayebanwa na masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, bali pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha za Serikali (PAC). Kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu, mojawapo ya majukumu ya PAC ni kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika Wizara na Mashirika ya Umma yaliyoainishwa katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. NSSF na TANAPA ni baadhi tu ya Mashirika ya Umma yaliyo chini ya usimamizi wa kibunge wa PAC.

Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zitto Kabwe, kwa kutumia makampuni yake ya Leka Dutigite Ltd. na Gombe Advisors Ltd., amefanya biashara na TANAPA, shirika la umma analolisimamia kama Mbunge na Mwenyekiti wa PAC. Mheshimiwa Zitto Kabwe na wanamuziki washirika wake, kwa kutumia makampuni ya Gombe Advisors Ltd. na Leka Dutigite Ltd., wamelipwa fedha za umma za TANAPA na NSSF.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo juu ya madai ya ukiukwaji wa Sheria uliofanywa na viongozi wa umma na mashirika ya umma katika kashfa hii. Pamoja na maelezo yatayotolewa , Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum juu ya matumizi ya fedha zilizotolewa na TANAPA na NSSF; msukumo uliofanya fedha hizo zitolewe na matumizi ya fedha hizo kwa kuzingatia masharti yanayosimamia fedha za umma na utawala bora katika usimamizi wa fedha za umma. Aidha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ifanye uchunguzi juu ya malipo na matumizi husika kwa kurejea masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Sheria nyingine zinazohusika. Kwa upande mwingine, kwa kuwa suala hili linahusu mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusika na usimamizi wa fedha za umma, Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge nayo ifanye uchunguzi wake juu ya madai ya masharti ya Katiba ya Nchi, Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na Kanuni za Bunge juu ya maadili ya kiongozi wa umma ikiwemo yahusuyo utangazaji wa maslahi.

Mheshimiwa Spika; Mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inatoa rai kwa wanamuziki na wasanii wengine wote nchini kuwa waangalifu na watu wanaotaka kutumia umaarufu wao kama wanamuziki na wasanii kwa lengo la kufanikisha dili za kifisadi. Bila kuchukua tahadhari ya kutosha, wasanii hao wanaweza kujikuta wakipoteza sifa na umaarufu wao ambao wameujenga kwa jitihada zao wenyewe.

Zitto Kabwe kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii amepost ujumbe huu usiku wa Mei 29 ambao unaonyesha kuwa na majibu juu ya maswali yaliyoulizwa na kambi ya upinzani juu ya umiliki wa Lekadutigite na Gombe Advisors,Hii ndiyo status yake.

Maelezo yangu kuhusu kazi za Kigoma AllStars/LEKADUTIGITE kwa NSSF na TANAPA.

Leo tarehe 29 Mei, 2014 Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu Habari, Michezo, Vijana na Utamaduni amenituhumu kuhusika na kinachoitwa ufisadi katika Shirika la TANAPA na NSSF.

Nasikitika kwamba katika hali niliyonayo ya kumwuguza mama yangu naingizwa kwenye siasa za majitaka. Kwa sasa nitatoa maelezo kwa ufupi ili kuondoa upotoshaji.

Kampuni ya LekaDutigite inamilikiwa na wasanii 15 ambapo kila mmoja ana hisa 5% ambazo niliwalipia ili waweze kushirikiana katika kazi zao. Hisa 25% zilizobakia zinamilikiwa na kampuni ya Gombe Advisors ambayo ni kampuni isiyofanya faida (Company limited by guarantee) na haina maslahi yeyote ya kibiashara (not for profit company). Hivyo Mimi binafsi sina maslahi yeyote ya kifedha zaidi ya kuwasaidia wasanii hawa katika kazi zao mbalimbali.

Wasanii wa Kigoma AllStars wamefanya kazi na TANAPA na NSSF, kazi ambazo zinajulikana na zipo. Kwa upande wa TANAPA wasanii hawa waliandaa kazi ya kuitangaza Hifadhi ya Saadani na walilipwa. Kwa upande wa NSSF wasanii hao walitunga wimbo na video yake na wimbo huo unatumika katika Shirika hilo.
Vile vile walifanya matamasha mbalimbali ya kuhamasisha watu kujiunga na NSSF. Wasanii wa Kigoma All Stars wote ni wanachama wa Mfuko huo.

Katika kazi zote hizi Mimi binafsi sijafaidika kwa namna yeyote ile kifedha. Kauli yeyote ya kujaribu kuonyesha kazi hizi za wasanii ni ufisadi ni kauli za kusikitisha na kukatisha tamaa kwa mtu ambaye anajaribu kusaidia wasanii kufaidika na kazi zao za sanaa.

Katika kazi zote hizi Mimi binafsi sijafaidika kwa namna yeyote ile kifedha. Kauli yeyote ya kujaribu kuonyesha kazi hizi za wasanii ni ufisadi ni kauli za kusikitisha na kukatisha tamaa kwa mtu ambaye anajaribu kusaidia wasanii kufaidika na kazi zao za sanaa.

Toka mwaka 2012 nilipoanza kujitokeza kusemea wasanii watu kadhaa wenye maslahi na tasnia hii wamekuwa wakinikatisha tamaa na hata wengine kuona nimewaingilia kazi zao.
Hivi sasa wasanii wa Kigoma AllStars ni wanahisa katika kampuni ya PERA Africa limited ili kufaidika na biashara ya miito ya simu. Yote haya nilifanya kwa uchungu nilionao kwa vijana wetu na sio kwa kutaka kufaidika kifedha. Nimeumizwa sana na tuhuma hizi za kuokoteza okoteza.

Inaniumiza zaidi kutokana na ukweli kwamba ninamwuguza mama yangu mzazi, kipindi ninachohitaji kutiwa moyo na kuombewa hata na maadui zangu kisiasa. Kipindi ambacho mama yangu yupo mahututi, tena mjumbe wa kamati kuu ya chama ambacho watoa tuhuma wanatoka, pole ninayopewa ndio hiyo. Hakuna namna ya kukosa ubinaadamu zaidi ya hivi.

Najua wajibu wangu ni kusimamia Mashirika ya Umma na nikiwa mpigania uwajibikaji nipo makini sana kuhakikisha sina mgongano wa maslahi katika mambo yangu. Ndio maana sina biashara yeyote ile ili kuhakikisha natimiza wajibu wangu kwa uadilifu mkubwa. Napata ‘moral authority’ ya kutaka uwajibikaji kwa sababu nafanya kazi zangu kwa misingi hiyo ‘at arms length’.

Hivyo ninataka mara moja CAG afanye ukaguzi wa kazi za wasanii hao kwenye NSSF na TANAPA. Pia achunguze kama Gombe Advisors ( company limited by guarantee) ina maslahi yeyote ya kifedha katika kazi hizo za wasanii. Nataka pia Shirika la NSSF na TANAPA waweke wazi mchakato wa kazi zao na wasanii hawa kupitia LEKADUTIGITE Limited.

Zitto Kabwe
Mei 29, 2014
Dar Es Salaam.
Share this article

0 comments:

ASANTE KWA KUTEMBEA BLOGU YAKO::KARIBU SANA

Toa Mani yako Hapa usiogope Tuko Pamoja

Post a Comment

 
Copyright © 2014 Chopa News • All Rights Reserved.
| Template Design by Anga Zio Team • Powered by Blogger online
back to top