Tuesday, August 26, 2014

TUSITEGEMEE MABADILIKO MAKUBWA KATIKA KATIBA MPYA.


Nianze kwa kumshukuru Mungu muumba mbingu na dunia na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana.

Baada ya kusema hayo nijitetee kuwa mimi siyo mtabiri lakini kuna kila dalili kwamba mabadiliko mengi yaliyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba yakigusa miundo ya taasisi nyeti za umma yatawekwa kando na huenda Bunge Maalum likatoa katiba isiyokuwa na mabadiliko makubwa kama ilivyotarajiwa.

Nasema hivyo kwa sababu kamati nyingi za bunge hilo zimebadili mapendekezo mengi hasa yanayowagusa viongozi na taasisi nyeti kama bunge, tofauti na ilivyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Jaji Joseph Warioba (pichani).

Miongoni mwa mambo ambayo yamependekezwa kurejeshwa kama yalivyokuwa ni muundo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo kwa mujibu taarifa kutoka kwenye kamati mbalimbali, litaendelea  na muundo wa sasa unaowajumuisha wabunge kutoka Zanzibar.
Katika maelezo yake, Jaji Warioba alisema moja ya kero za muungano katika eneo la bunge ni malalamiko kwamba wabunge kutoka Zanzibar wamekuwa wakishiriki wengi katika Bunge la Muungano na hushiriki kujadili mambo yanayohusu Tanzania Bara.

Kupitia mfumo wa serikali tatu, rasimu ilikuwa na mapendekezo ya kuwapo kwa Bunge la Muungano lenye wabunge 75, lakini mapendekezo hayo pia yamefutwa katika kamati karibu zote na kurejesha mfumo wa sasa pamoja na uwepo wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Nilimsikia Mwenyekiti wa Kamati Namba Tano, Hamad Rashid Mohamed akisema wiki iliyopita kuwa suala la muundo wa bunge lilisababisha mvutano mkubwa katika kamati yake na baadhi ya wajumbe walikuwa wakihoji uwakilishi mkubwa wa wabunge wa Zanzibar katika Bunge la Muungano hata kwa mambo ya Tanzania Bara.

Hata hivyo, alitetea hali hiyo akisema uwepo wa wabunge kutoka Zanzibar ni moja ya masharti yaliyowekwa na katiba. Alisema mwaka 1964 mambo yote ya Tanganyika yaliingizwa kwenye Serikali ya Muungano lakini sasa  ni lazima kubainisha mambo ya muungano na ya Tanganyika.

Wapo Watanzania bara wanaouliza hivi wabunge 70 wanaokuja kutoka Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ni halali? Wengine wanakwenda mbali zaidi na kuhoji, iweje Zanzibar yenye watu chini ya milioni 1.3 iwe na wabunge wote hao na Dar es Salaam yenye watu zaidi ya milioni tatu iwe na wabunge chini ya 10?
Hoja ya ushiriki wa Wazanzibari katika masuala ya Tanzania Bara iliripotiwa pia kuibuka katika Kamati Namba Moja ambako mmoja wa wajumbe, Ally Keissy alinukuliwa akihoji sababu za wajumbe wa Zanzibar kushiriki mambo ambayo wao siyo yao.

Mbali na muundo wa bunge, kamati nyingi pia zimefuta mapendekezo kadhaa yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ambayo ni pamoja na wabunge kutokuwa mawaziri, ukomo wa ubunge kwa vipindi vitatu vya miaka mitano mitano, wabunge kuwajibishwa na wananchi, kupunguzwa kwa madaraka na kinga ya rais.

Katika Kamati Namba Tano, Hamad alithibitisha kuwa suala la wananchi kumuondoa mbunge lilikataliwa.
Alisema kuliweka jambo hilo katika katiba ni kuleta matatizo na kwamba wameliacha suala hilo mikononi mwa vyama vya siasa kuangalia kama mbunge anafanya kazi ya ilani zao au la. Kwa hiyo kifungu hicho kinabaki kama kilivyo sasa.

Ukweli ni kwamba kuwekwa kando kwa mapendekezo mengi yaliyolenga kurekebisha mifumo ya uongozi na utawala, kumesababisha mgawanyiko hasa miongoni mwa wajumbe watetezi wa muungano wa serikali mbili, ambao awali, waliahidiwa kwamba muundo huo usingekuwa na sura yake ya sasa, bali ungeboreshwa.

Wapo wanaodai kuwa kufanyia marekebisho kutawapa wapinzani sifa maana umma utaamini kwamba bila wao hakuna kinachoweza kubadilika, haya ni mawazo potofu sana kwa sababu katiba inayoandikwa si ya chama fulani au kundi.

Kama tutarejesha kila kitu ambacho kiko kwenye katiba tuliyonayo kuna maana gani ya kuwa na mchakato wa katiba mpya?

Wote tunajua kuwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliamua kupinga mapendekezo ya serikali tatu na kutaka tubaki na muundo wa serikali mbili zilizoboreshwa, lakini hayo maboresho hatuoni.
Kwa hiyo wananchi wataamini kwamba kilichosemwa na Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi), ni cha kweli, hilo ni angalizo langu. Ni vyema sana kutafakari mambo ya msingi badala ya kung’ang’ania itikadi za vyama.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.


HATA KUBONYEZA KA Like Tu Hapo JUU HUTAKI; BONYEZA BASI MPEDWA

JIONEE BAADHI TU YA MAMBO WAFANYIWAYO MABINTI WAENDAO COCO BEACH HAPA......

PIA ISOME NA HII HAPA CHINI INAKUHUSU

Share this article

0 comments:

ASANTE KWA KUTEMBEA BLOGU YAKO::KARIBU SANA

Toa Mani yako Hapa usiogope Tuko Pamoja

Post a Comment

 
Copyright © 2014 Chopa News • All Rights Reserved.
| Template Design by Anga Zio Team • Powered by Blogger online
back to top