Monday, June 30, 2014

Evans Elieza Aveva ashinda Uraisi wa Simba SC.


Evance Aveva akishukuru baada ya kutangazwa kuwa Rais mpya wa klabu ya Simba na kuchukua mikoba ya Ismail Aden Rage, aliyemaliza muda wake wa miaka minne.
Amin Bakhresa akitangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Simba SC.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe jana aliokoa jahazi baada ya kutoa Sh. milioni 20 na kuwezesha kufanyika kwa mkutano mkuu wa uchaguzi wa uliomweka madarakani Evans Aveva.

Hanspoppe alitoa fedha hizo ili kugharamia uchaguzi baada ya kampuni ya bia Tanzania (TBL), ambao ndiyo wadhamini wa klabu hiyo ambao waliahidi kugharamia mkutano huo kushindwa kufanya hivyo kwa wakati.



Habari za ndani zilidai kwamba, rais aliyemaliza muda wake, Ismail Aden Rage alitaka uchaguzi usifanyike kutokana na wadhamini kutotoa fedha hizo.

Hata hivyo, uchaguzi huo uliohudhuriwa na wanachama 2,501 ulifanyika kama ilivyotarajiwa huku Aveva akionekana kukosa upinzani kutokana na kuenguliwa na Kamati ya Uchaguzi kwa aliyekuwa mpinzani mkubwa, Michael Wambura.

Mpinzani aliyesalia wa Aveva, Andrew Tupa hana umaarufu wa kutosha katika klabu hiyo na hivyo kumuacha Aveva katika mbio zilizoonekana za “farasi mmoja”.

Nafasi ya makamu rais ilikwenda Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ aliyemshinda Swedi Mkwabi na Jamhuri Kihwelu ‘Julio’.Mkutano wa uchaguzi huo ulifunguliwa kwa dua maalum saa 4:49.

Wambura alikumbana na balaa jingine baada ya kuzuiwa kuingia katika mkutano huo.Wakati huo huo, wakati kocha mkuu wa klabu ya Simba, Zdravko Logarusic, akisema hajui atarejea lini nchini, Kamati ya Usajili iko katika hatua ya mwisho kumnasa mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uganda, Hassan Waswa.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam, Simba iko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa Waswa ili kuongeza nguvu kwenye safu yake ya ushambuliaji.

Chanzo kilisema kuwa leo baada ya uongozi mpya kuingia madarakani utafanya maamuzi ya mwisho ya kuona ni wachezaji wangapi watabaki kuichezea Simba katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayoanza kutimua vumbi Agosti 24 mwaka huu.

“Logarusic anatua keshokutwa (leo) na yeye ndiye ataamua lini mazoezi yaanze rasmi…sisi kazi yetu ya kuimarisha timu tumeifanya kikamilifu licha ya kukutana na changamoto iliyohusicha uchaguzi mkuu,” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hanspoppe Zacharia.

Hata hivyo, Loga alisema jana kuwa hajui atakuja lini nchini kwani bado hajapata taarifa zozote kutoka kwa Hanspoppe, hivyo anasubiri taarifa hizo.

Logarusic ambaye mkataba wake wa awali wa miezi sita ulimalizika Mei 31 mwaka huu anatarajiwa kuendelea kuliongoza benchi la ufundi la Wekundu wa Msimbazi akisaidiwa na nahodha wa zamani wa timu hiyo, Selemani Matola.

Simba ilimaliza msimu uliopita ikiwa katika nafasi ya nne na kukosa tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwa mwaka wa pili mfululizo.

 BAADA YA UCHAGUZI



Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva.

ASIYEPENDA kusikiliza maoni ya watu, akaamini anajua kuliko mtu yeyote, mara nyingi huishia kufeli, kuna mifano ya watu wengi sana.

Lakini katika kusikiliza, si lazima kila unaloambiwa ulifanyie kazi, kwa kuwa kuna maoni ambayo yanaweza kuwa si sahihi, ukisikiliza kila uliloambiwa na kuliamini, pia unaweza kufeli.

Ndiyo maana Wanasimba wakamuamini Evans Elieza Aveva na kumpa urais kwa kuwa wanajua ana uwezo wa kuikwamua klabu yao kutoka kwenye matatizo, migogoro, kashfa kibao za uuzaji wachezaji bila ya kupata fedha na mengine mengi.

Pamoja na malumbano kwa zaidi ya mwezi kuhusiana na uchaguzi mkuu, hatimaye wanachama wa Simba, jana waliamua kumpa Aveva dhamana ya kuiongoza klabu yao hiyo ambayo inahitaji mabadiliko ili kurudi kwenye maendeleo na sifa yake kwa kuwa Simba ni klabu maarufu barani Afrika na yenye mafanikio katika nyanja za kimataifa kwa hapa nyumbani.

Simba imekuwa kwenye utulivu kwa miaka mingi, kabla ya uongozi wa ‘uncle’ Ismail Aden Rage, haujaingia madarakani ambao katika miaka minne ni mwaka mmoja tu ulikuwa una mafanikio, baada ya hapo ni migogoro, uadui na matatizo lukuki.

Matatizo yaliyoondoa umoja ndiyo yaliyoifanya Simba kupoteza sifa yake ya sharubu imara na badala yake karibu kila timu, zikiwemo hata Mbeya City iliyopanda daraja, zikaanza kuisumbua, kuifunga na hata ukipenda unaweza kusema waliionea Simba.

Simba haikuwa Simba tena, ndiyo maana wakati Wanasimba wanakupa kura, wengi wao watakuwa wanataka mengi lakini mawili furaha ya moyo, yaani kuwa na timu inayoshinda na maendeleo ya klabu, vitakuwa ni vitu vya kwanza kabisa.

Vipande:

Simba imevunjika vipande, kipindi cha Rage kilikuwa cha hovyo, watu hawakuwa na upendo, hawakuelewana na mwisho kila mmoja akaishi kwa kuangalia maslahi yake na si yale ya Simba tena.
Ndiyo maana uliona Simba ilivyoyumba, kwa kuwa kila mmoja aliigeuza chukua chako mapema, hivyo una kazi ya kuzuia hilo na badala yake kila mmoja afanye kwa maslahi ya klabu.

Siri:

Inawezekana watakaosoma makala haya, wataelewa lakini siri itabaki kuwa ya kwako kwamba siku zote msemakweli, anachukiwa.
Wala usisimame, songa mbele kama utakuwa unafanya mambo kwa ajili ya maslahi ya klabu. Pia ningekushauri hata kama utakuwa unajua mambo mengi ya klabu hiyo kuliko mimi, usikubali kupendwa sana.

Nimeona viongozi wengi wanaoingia madarakani wamekuwa wakipenda sana kuonekana watu wazuri wanaotaka kumfurahisha kila mtu, ni kosa kubwa.
Kama kuna mtu au kundi la watu linaharibu, basi waeleze ukweli kwa nia na njia nzuri na mwisho lengo liwe umoja na kusaidia kuijenga Simba.
Umoja:

Kama nilivyoeleza awali, Simba ya sasa iko katika vipande. Moja ya kazi kubwa ni kuunganisha makundi makubwa ambayo chuki zao ni zile za kibinadamu na zinaiumiza Simba.
Najua hauwezi ukafanya mambo yote kwa wakati mmoja, lakini umoja ni kati ya mambo ya mwanzo kabisa kuanza kuyafanya kwa kuwa bila ya kuwa pamoja hakuna kitu kimoja kinaweza kuwa cha umoja na kushika namba moja.

Binadamu wana kawaida ya kusahau, huenda wako waliokuwa na hasira kwa kuwa walitaka kugombea wakaondolewa, wengine wana hasira kwa kugombea na kushindwa. Lakini wote hao ni Simba na wana uwezo wa kuisaidia klabu yao.

Hivyo Aveva, una kazi kubwa ya kuwaunganisha Wanasimba hata kama itakuwa ni taratibu huku ukiendelea kufanya mambo mengine ya mafanikio.
Simba ni kubwa, kwa hali iliyokuwa imefikia, haiwezi kubadilika ndani ya siku mbili na kila kitu kikaenda tofauti. Lazima muda wa kutosha unatakiwa.

Lakini hakuna mabadiliko yatakayopatikana kwa siku moja bila ya kuanza taratibu. Hivyo ni vizuri kuanza taratibu kuwaunganisha Wanasimba kwa ajili ya kujenga Simba moja imara kuliko ‘visimba’ vingi visivyokuwa na ushirikiano na mwisho ni kuiua tu nguvu ya klabu hiyo.

Najua utakuwa na kazi kubwa sana, karibu usaidie kuendeleza soka na kama kawaida, ukipatia tutakumwagia sifa za kutosha, lakini siku ukikosea, basi ukweli ndiyo ada.



Bonyeza Like hapo juu uwe wa kwanza kupata habari mpya.

Share this article

0 comments:

ASANTE KWA KUTEMBEA BLOGU YAKO::KARIBU SANA

Toa Mani yako Hapa usiogope Tuko Pamoja

Post a Comment

 
Copyright © 2014 Chopa News • All Rights Reserved.
| Template Design by Anga Zio Team • Powered by Blogger online
back to top