Monday, June 30, 2014

Binti wa darasa la 7 alawitiwa na Vijana watatu huko Pwani, Mlezi wake apewa laki mbili kama kifunga Mdomo.

Denti wa kike wa darasa la saba anayesoma katika Shule ya Msingi Chanzige B iliyopo Kisarawe, Pwani aliyefanyiwa unyama wa kulawitiwa na vijana watatu.

INASIKITISHA sana! Denti mmoja wa kike wa darasa la saba anayesoma katika Shule ya Msingi Chanzige B iliyopo Kisarawe, Pwani amejikuta katika wakati mgumu baada ya kulawitiwa na kusababishiwa maumivu makali sehemu zake za siri.
Simulizi ya binti huyo inayouma sana, inaeleza kuwa denti huyo alifanyiwa unyama huo na vijana watatu ambao bado hawajafahamika majina yao mara moja lakini amekuwa akimtaja mmoja kwa jina la Musa.
Tukio hilo lenye sura ya majonzi hasa kwa wazazi na watoto, lilitokea hivi karibuni Kisarawe mkoani Pwani lakini ilifanywa siri kwa muda mrefu na mtoto huyo kukaa bila matibabu.
Chanzo chetu cha habari kinasema kuwa, shangazi wa mtoto huyo ambaye anaishi naye ndiye sababu ya kutopata tiba, kwani anadaiwa kuchukua kiasi cha shilingi 200,000 kutoka kwa Musa anayetajwa kuwa mmoja wa wahusika kama kifunga mdomo.

“Haya mambo yametokea muda tu na huyo mtoto (anamtaja jina lakini linahifadhiwa) alimwambia shangazi yake kuwa huyo Musa na wenzake wanahusika, lakini cha ajabu walikutana huko na kupeana hizo fedha ili mambo yaishe.
“Hii haikubaliki kabisa. Unajua huyo shangazi mtu anafanya hivyo kwa sababu si mwanaye, ingekuwa ni damu yake kweli asingeweza kufanya kitu cha namna hiyo,” kilipasha chanzo hicho na kuongeza:“Ilibaki kidogo mtoto ashindwe kufanya mtihani wake wa Mock kwa sababu ya tukio hilo. Kiukweli si jambo la kulifumbia macho. Huyo mama (shangazi) anatakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria.”

Chanzo hicho kikazidi kusema kuwa, awali kesi hiyo ilifikishwa katika Kituo cha Polisi Kisarawe na kufunguliwa jalada lakini shangazi wa mtoto huyo aliamua kuyamaliza mambo hayo na mmoja wa watuhumiwa baada ya kupewa kiasi hicho cha fedha.
Uchunguzi wa Amani umegundua kuwa, sakata hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi Kisarawe na kufunguliwa jalada nambari KIS/RB/326/2014, ambapo Fomu ya Polisi Nambari 3 (PF3) ilitolewa kwa ajili ya matibabu ya mtoto huyo.

Akisimulia zaidi, mama mzazi wa mwanafunzi aitwaye Mariam Said alisema, alipata taarifa za mwanaye kukumbwa na masahibu hayo ambapo aliamua kusafiri kutoka Mlandizi anapoishi hadi Kisarawe kufuatilia tukio hilo.

“Inaniuma sana mwanangu kufanyiwa unyama halafu mambo yanamalizwa kienyeji. Nilikuja hadi hapa, nikamwuliza shangazi yake na binti yangu juu ya tukio hilo, akakiri lakini akasema eti mwanangu hakuwa mkweli mapema.
“Nikaamua kwenda polisi mimi na ndugu zangu wengine. Tulipouliza hiyo kesi kituoni hapo, tukaambiwa ni kweli ilifungiliwa na nikatajiwa RB (ile iliyoandikwa hapo juu). Polisi wakatuambia, walishangaa kuona mlalamikaji harudi tena na hata PF3 waliyotoa haikurudishwa tena baada ya kuondoka,” alisema Mariam.

Binti huyo alisema alifanyiwa ukatili huo wakati akitokea shuleni na kwamba alimweleza shangazi yake kila kitu kuhusiana na tukio hilo kabla ya kwenda naye polisi kutoa taarifa.
“Baada ya hapo tulikwenda katika Hospitali ya Kisarawe lakini sikupata matibabu kwa sababu shangazi alisema hana pesa ya malipo, kukarudi nyumbani na kununua dawa kwenye maduka ya dawa,’’ alisema mtoto huyo na kuongeza:
“Pale hospitalini, shangazi alitakiwa kutoa kadi ya Bima au shilingi 10,000 ili nitibiwe. Sasa hakuwa na Bima wala hiyo pesa ndiyo maana ikashindikana.”


Gazeti hili lilifunga safari hadi Shule ya Msingi Chanzige B na kuzungumza na Mwalimu Mkuu, Issac Eliah ambaye alikiri kupokea taarifa ya mwanafunzi wake kubakwa na kulawitiwa kutoka kwa shangazi wa mtoto huyo na kutoa ruhusa kwa ajili ya matibabu.
Shangazi wa mtoto huyo alipotakiwa kuzungumzia ishu ya kuzima kesi hiyo kwa madai ya kupewa shilingi 200,000 alisema: “Mimi sitaki kuzungumzia suala hilo, nendeni polisi mkaulize siyo kuniuliza mimi.”
Chanzo:http://mdadisibongo.blogspot.com/

Bonyeza Like hapo juu uwe wa kwanza kupata habari mpya.

Share this article

0 comments:

ASANTE KWA KUTEMBEA BLOGU YAKO::KARIBU SANA

Toa Mani yako Hapa usiogope Tuko Pamoja

Post a Comment

 
Copyright © 2014 Chopa News • All Rights Reserved.
| Template Design by Anga Zio Team • Powered by Blogger online
back to top