Tuesday, October 14, 2014

MAKONGORO MAHANGA: POLISI JAMII NDIYO DAWA YA ‘MBWA MWITU NA PANYA ROAD’.

MATATIZO YA WANANCHI
Wananchi wa Segerea waliozungumza na Uwazi, walibainisha matatizo mbalimbali yanayowakabili, yakiwemo vitendo vya ukabaji na uporaji unaofanywa na makundi ya vijana wadogo, maarufu kama Mbwa Mwitu na Panya Road, ukosefu wa huduma bora za kijamii zikiwemo maji safi na salama, madawa kwenye vituo vya afya, zahanati na hospitali, ukosefu wa vifaa vya kutosha vya kufundishia kwenye shule za msingi na sekondari na ubovu wa miundo mbinu ikiwemo barabara na madaraja.

MAELEZO YA MBUNGE
Baada ya kuzunguka kwenye kata zote nane za jimbo hilo, Uwazi lilimtafuta mbunge wa jimbo hilo, mheshimiwa Makongoro na kufanikiwa kumpata ofisini kwake, kwenye makutano ya Barabara za Bibi Titi na Morogoro ambapo alikuwa na maelezo yafuatayo.

1. VITENDO VYA UHALIFU
Akizungumzia suala la ukosefu wa ulinzi na usalama, Makongoro alikiri kuwepo kwa tatizo hilo linalowasumbua wananchi lakini akasisitiza kwamba kwa kuwa vijana wanaofanya uhalifu huo wanaishi ndani ya jamii, hakuna njia nyepesi ya kukabiliana nao zaidi ya jamii yenyewe kuamua kulivalia njuga suala hilo.

“Ni rahisi sana kama wananchi wataamua wenyewe na ndiyo maana mara kwa mara nimekuwa nikifanya mikutano ya hadhara jimboni kwangu kwa kushirikiana na jeshi la polisi, kuwaelewesha wananchi juu ya umuhimu wa suala la ulinzi shirikishi au kama wengine wanavyoita, polisi jamii.

“Nawaomba wananchi wa Segerea wakubali kushirikiana na serikali na jeshi la polisi kwa kushiriki kikamilifu katika suala zima la ulinzi na usalama. Kote ambako polisi jamii inafanya kazi, vitendo vya kihalifu vimepungua sana.

2. HUDUMA ZA KIJAMII
“Nimekuwa madarakani kwa kipindi kirefu na katika muda huo, nimefanikiwa kuzipunguza sana kero za wananchi wangu hususan katika suala la huduma za kijamii. Kuna zaidi ya shule za msingi 50 jimboni mwangu na za sekondari 13.

“Kati ya hizo, ni chache sana ambazo bado zina matatizo ya ukosefu wa madawati na vifaa vya kufundishia lakini nyingi  zina mazingira na vifaa vya kutosha vya kufundishia. Suala la maabara ndiyo tunahangaika nalo kwa sasa.

“Kuhusu suala la afya, kata zote nane zina zahanati, nyingine zipo mbili katika kata moja ingawa bado matatizo yapo kwenye kata za Kipawa ambako ujenzi bado unaendelea na Kata ya Kimanga ambako nikiri kwamba kuna matatizo. Zahanati zote zimejengewa uwezo wa kuwazalisha akina mama wajawazito na lengo ni kuhakikisha zote zinafanya kazi saa ishirini na nne.

“Changamoto kubwa ni upatikanaji wa dawa na nyumba za madaktari ambapo hili linasababishwa na serikali kuu. Tukija kwenye suala la maji, ni kweli kumekuwa na tatizo kubwa la uhaba wa maji jimboni kwangu lakini kama mbunge, nimejitahidi kuchimba visima sehemu mbalimbali kupunguza tatizo.

“Hivi sasa kuna mradi mkubwa wa maji ya Mto Ruvu ambao unaelekea kukamilika, nawaahidi wananchi kwamba ukikamilika, suala la matatizo ya maji Segerea litabaki kuwa historia.

“Kwa upande wa miundombinu, hakuna jimbo ambalo lilikuwa na barabara mbovu kama Segerea lakini nimejitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu hivi sasa karibu barabara zote jimboni mwangu zipo katika kiwango cha lami.

“Nyingine zilishakamilika kwa mfano ya kutoka Tabata, Segerea, Majumba Sita hadi Vingunguti imejengwa kwa kiwango cha lami. Pia daraja la Vingunguti limekamilika na Barabara ya Segerea kuelekea Kinyerezi nayo ipo kwenye hali nzuri kabisa. Daraja la Majumba Sita lilikuwa dogo lakini limetanuliwa.

“:Barabara ya Tabata Dampo kuelekea Kigogo inajengwa kwa kiwango cha lami, pia Kinyerezi kuelekea Malamba Mawili hadi Kifuru ujenzi unaendelea.

“Kimsingi najitahidi sana kuhakikisha wananchi wa Segerea wanaishi maisha mazuri ingawa kuna wanasiasa ambao kazi yao ni kunigombanisha na wananchi wangu mpaka wengine wanakuwa wanazomeazomea. Hata hivyo, hawanikatishi tamaa nitaendelea kuwatumikia wananchi wa Segerea,” alihitimisha Makongoro.

ANGALIA PICHA MBALIMBALI ZA SHEREHE YA KUZALIWA MAPACHA WA MENGI.


HATA KUBONYEZA KA Like Tu Hapo JUU HUTAKI; BONYEZA BASI MPEDWA
PIA ISOME NA HII HAPA CHINI INAKUHUSU

Share this article

0 comments:

ASANTE KWA KUTEMBEA BLOGU YAKO::KARIBU SANA

Toa Mani yako Hapa usiogope Tuko Pamoja

Post a Comment

 
Copyright © 2014 Chopa News • All Rights Reserved.
| Template Design by Anga Zio Team • Powered by Blogger online
back to top