Saturday, July 5, 2014

Ngassa, Mbuyu wamtibua Maximo Jana Mazoezini.

 Mshambuliaji wa Yanga SC, Mrisho Ngassa.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbrazili, Marcio Maximo, jana aligeuka mbogo katika mazoezi ya timu hiyo, baada ya nyota Mrisho Ngassa na Mbuyu Twite kutotokea mazoezini na wakatumia simu kutoa taarifa, jambo ambalo kocha hakupendezwa nalo.
Yanga jana ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola, Mabibo, ambapo nyota hao walikosekana na ilisemekana kuwa walishindwa kuhudhuria mazoezi kwa kuwa walikuwa wanaumwa, licha ya juzi Alhamisi jioni kuwepo mazoezini.

Beki wa kimataifa wa Yanga, Mbuyu Twite.

Maximo alisikika akiwaka wakati akiongea na wachezaji baada ya
 xmazoezi ambapo alikuwa akihimiza umoja huku akisema kuwa mchezaji yeyote ambaye anajihisi kuumwa, anatakiwa kufika mazoezini na kumweleza daktari na siyo mchezaji kupiga simu akiwa nyumbani.

“Mazoezi ya leo yameenda vizuri, kila mmoja anaonekana kufuata maagizo yangu, lakini kitu kimoja cha msingi lazima timu iwe na umoja na umoja wenyewe ni kuwa karibu na kufahamiana kwa wachezaji.
“Hakuna asiyejua Malaria kuwa ni ugonjwa mbaya siyo Tanzania tu, popote pale, lakini kwa timu ambayo inataka kujenga umoja lazima mchezaji afike uwanjani na kumweleza daktari, siyo hili la kutuma taarifa mtu akiwa nyumbani.

Kocha Mkuu wa Yanga, Marcio Maximo.

“Mtu kama anaumwa anatakiwa kuja mazoezini na kutoa taarifa zake,” alisema Maximo.
Mazoezi ya timu hiyo, yanatarajiwa kuendelea leo Jumamosi katika Ufukwe wa Agakhan asubuhi tu na jioni ni muda wa kupumzika. Yanga walianza mapema mazoezi, kujiwinda na michuano ya kimataifa ya Kombe la Kagame na Ligi Kuu Tanzania itakayoanza Agosti 24, mwaka huu.

Katika hatua nyingine Maximo, ameanza kumkubali ‘mbaya’ wake wa zamani, kipa Juma Kaseja kutokana na juhudi binafsi ambazo ameendelea kuzionyesha katika mazoezi.
Katika mazoezi ya jana kwenye Uwanja Shule ya Sekondari ya Loyola iliyopo Mabibo, Kaseja alizidi kumkosha Mbrazili, baada ya kupangua mashuti makali mawili yaliyopigwa na moja likipigwa na straika Hussein Javu.

Kitendo cha Kaseja kupangua mashuti hayo, kilimfurahisha Maximo ambapo alimpigia makofi kuashiria kumkubali, huku akitamka maneno: “Safi sana Kaseja, safi sana...” lakini baadaye alimpumzisha.
Pia Maximo amewahimiza wachezaji wa timu hiyo kuzingatia mazoezi katika siku hizi mbili za mapumziko na siyo kuendekeza starehe ‘disco’.
Maximo alisikika akiwahimiza kutotumia mapumziko kwenda disco na kwenye Bongo Fleva, badala yake kutilia maanani kile walichovuna mazoezini.
“Jioni (jana) hatutafanya mazoezi lakini isiwe ndiyo muda wa kwenda katika starehe, msingi wa mchezaji ni kufikiria nini cha kufanya uwanjani na si vinginevyo,” alisikika Maximo akiwaasa ‘wanafunzi’ wake.


Bonyeza Like hapo juu uwe wa kwanza kupata habari mpya.

Share this article

0 comments:

ASANTE KWA KUTEMBEA BLOGU YAKO::KARIBU SANA

Toa Mani yako Hapa usiogope Tuko Pamoja

Post a Comment

 
Copyright © 2014 Chopa News • All Rights Reserved.
| Template Design by Anga Zio Team • Powered by Blogger online
back to top