MWANAMKE mmoja kikongwe, Rebeka Shija mwenye umri wa miaka 82, mkazi wa Kata ya Nyahanga, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, ameuawa kikatili kwa kukatwa na shoka kichwani na mke wa mtoto wake aitwaye Magreth Richard, saa tatu asubuhi Juni 24, mwaka huu.
Kwa mujibu wa mmoja wa wanafamilia ya marehemu aliyekataa kutajwa gazetini, alisema mwanamke huyo alikwenda nyumbani kwa mtoto wake wa kiume, Bundala Sengasenga (46) baada ya kuitwa na mke wa mwanaye akidai kusaidiwa kuanika dengu.
Inadaiwa kuwa chanzo cha mauaji hayo kina uhusiano mkubwa na masuala ya kishirikina, kwani Novemba mwaka jana, familia hiyo ilipoteza mtoto mdogo aliyefariki katika mazingira ya kutatanisha baada ya kutumbukia katika kisima nyumbani kwao, kitu kilichosababisha wanafamilia kuanza kutuhumiana uchawi.
Katika msiba huo, kikongwe huyo alionekana kushtukia kifo hicho baada ya mama yake mzazi, ambaye ndiye anayedaiwa kumpiga shoka bibi huyo, kumgundua mwanaye kuwemo kisimani usiku wa saa nne, licha ya ukweli kwamba alianza kutafutwa tokea saa nane mchana.
Ilielezwa kuwa kabla ya tukio la juzi, Magreth alikwenda kwao Kata ya Zongomera ambako alikaa kwa muda wa siku nne na aliporudi, siku mbili baadaye ndipo alipofanya unyama huo.
Inadaiwa mara baada ya mumewe kuondoka kwenda mashambani kwao huko Lugela, Magreth alikwenda katika grosari moja iliyo jirani na kuanza kunywa pombe kali aina ya viroba.
Alipomaliza kunywa, alikwenda nyumbani kwa shemeji yake na kumuomba bibi huyo kwenda kumsaidia kuanika mazao yake. Kabla ya kufika kwake, alipita kwa jirani yake Mzee Noel Mkisi na kuazima shoka, alilodai ni kwa ajili ya kuchanja kuni.
Dakika 15 baadaye inadaiwa ilisikika sauti ya mayowe na alipotumwa mwanamke mmoja kuulizia kulikoni, Magreth aliwaeleza kuwa marehemu alidondoka karibu na sufuria na kwamba alitokwa damu, lakini watu walipofika walimkuta ameanguka ukumbini akiwa na majeraha mawili kichwani ya shambulio la kitu kizito chenye ncha kali.
Magreth aliwaambia watu kuwa mama mkwe wake alifikia sebuleni wakati yeye akiwa nje, alimwona mtu ambaye hakuweza kumfahamu akitoka sebuleni hapo na kukimbia ndipo alipoangalia na kumkuta ameanguka huku akitapatapa.
Aidha, alionekana kubabaika alipoulizwa sababu ya kuazima shoka, damu kutapakaa kifuani na kwenye karo la maji, akidai alikuwa katika siku zake, majibu ambayo yaliwashangaza watu. Shoka hilo lilipatikana baadaye likiwa katika shimo la taka baada ya polisi kunyonya maji machafu yaliyokuwepo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Kihenya Kihenya, alisema marehemu aliuawa kwa kukatwa shoka kichwani na mtuhumiwa huyo anashikiliwa.
Kamanda Kihenya alisema mtuhumiwa baada ya kufanya mauaji hayo, alimuacha marehemu sebuleni na kwenda kutumbukiza shoka alilotumia kwenye maji na kuongeza kuwa kitendo hicho kinahusishwa na imani za kishirikina.
0 comments:
ASANTE KWA KUTEMBEA BLOGU YAKO::KARIBU SANA
Toa Mani yako Hapa usiogope Tuko PamojaPost a Comment