Taarifa hizo zilipokelewa kwa shangwe na wananchi wa jimbo hilo kwani pia waliahidiwa kulipwa fidia nono. Wakatakiwa kuacha kuendeleza makazi yao ikiwemo kujenga nyumba mpya, kuzikarabati zilizopo, kuuza au kufanya shughuli zozote za kiuchumi.
Miaka ikazidi kuyoyoma, suala la kulipwa fidia nono likageuka na kuwa kizungumkuti, nyumba zikaanza kubomoka, ardhi ikawa haiuziki wala wananchi hawakopesheki kwa dhamana ya ardhi tena, sasa ni miaka 6 tangu kipindi hicho, hakuna kinachoeleweka.
Mizengwe hiyo ni miongoni mwa matatizo lukuki yanayowakabili wakazi wa jimbo hilo, ambapo gazeti hili liliyabaini.
Kupitia kolamu ya Jimbo kwa Jimbo, Uwazi lilifanikiwa kuzungumza na wakazi wa maeneo ya Toangoma, Kimbiji, Kongowe, Vijibweni, Kisarawe II, Tungi, Mbagala Rangi Tatu, Mianzini na maeneo mengine mengi ya jimbo hilo.
MATATIZO YA WANANCHI
Ukiachilia mbali suala la mgogoro kati ya wananchi na serikali kuhusu ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni, Uwazi limebaini uwepo wa matatizo mengine lukuki yakiwemo mgogoro wa ardhi katika maeneo ya Minondo, Amani Gomvu na Somangila.
Wananchi wa maeneo hayo waliliambia gazeti hili kwamba, wamebomolewa nyumba zao na kulipwa fidia kiduchu kwa madai ya kupisha ujenzi wa nyumba za askari, mchakato uliogubikwa na utata mkubwa kuanzia fidia mpaka kwenye zoezi lenyewe la ubomoaji lililofanyika usiku wa manane.
Pia wananchi wa jimbo hilo wanakabiliwa na matatizo ya ukosefu wa huduma za afya ambapo wengi wanalazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za uhakika katika Hospitali ya Temeke.
Uhaba wa walimu, madawati, vyumba vya madarasa na vifaa vya kufundishia pia ulibainika katika maeneo mengi jimboni humo. Uvuvi haramu wa kutumia baruti na sumu hasa maeneo ya Mjimwema, pia ulibainika kufanywa kwa wingi katika fukwe za Bahari ya Hindi jimboni humo na kuhatarisha maisha ya maelfu ya wakazi wa Jiji la Dar wanaotumia samaki kama kitoweo.
Yote tisa, kumi ilibainika kwamba baruti ambazo zikitengenezwa kienyeji zinalipuka kama mabomu zinauzwa kama karanga eneo la Feri, mita chache tu kutoka Ikulu. Hayo ni baadhi ya matatizo yanayowakabili wananchi wa jimbo hilo ambayo Uwazi liliyabaini.
Ili kupata mzani wa habari, Uwazi lilimtafuta mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Faustine Engelbert Ndugulile ambaye alikuwa na haya ya kusema:
MBUNGE NDUGULILE
1. MJI MPYA WA KIGAMBONI
Mheshimiwa Ndugulile alikiri kwamba mchakato wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni umekuwa msiba mzito kwa wananchi wa jimbo lake, akatupia lawama zake kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ‘kubabaisha’ mengi, ikiwemo kubadili viwango vya fidia wanayopaswa kulipwa wananchi mara kwa mara.
“Namshukuru Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye alisikiliza kilio cha wananchi wangu na kuamuru mchakato huo usimame.
2. UVUVI HARAMU
“Tunajitahidi sana kupambana nao. Kuna taasisi inaitwa BMU (Beach Management Unit) tunashirikiana nayo bega kwa bega kuzuia tatizo hilo.
Pia tumeunda vikosi vya ulinzi ufukweni tukisaidiana na askari wa kikosi cha majini lakini changamoto kubwa ni kwamba hakuna ufadhili wa fedha na vifaa vya kupambana na uhalifu huo,” alisema Ndugulile.
3. BOMOABOMOA MINONDO, SOMANGILA
Mheshimiwa Ndugulile alikiri kwamba ni kweli kuna tatizo lingine kubwa katika mradi wa nyumba za askari kwenye eneo la Minondo, Somangila na Amani Gomvu na kueleza kuwa wananchi wamebomolewa nyumba zao bila kulipwa.
“Wengine wamepewa fidia kiduchu ambazo hazilingani na thamani ya mali zao, Mkuu wa Mkoa (Said Mecky Sadick) ndiye anajua kila kitu kuhusu mwekezaji aliyefanya unyama huo kwa wananchi kwani siyo mradi wa serikali,” alisema Ndugulile.
3. HUDUMA MBOVU ZA KIJAMII
“Naijua adha wanayoipata wananchi wangu wanapohitaji huduma za kiafya, nimejitahidi kusimamia kupandishwa hadhi kwa Hospitali za Vijibweni na Rangi Tatu, pia zahanati ya Kimbiji imepanda hadhi na kuwa kituo cha afya.
“Nimefanikisha kupatikana kwa ambulance kwenye maeneo ya Hospitali za Kimbiji, Vijibweni na Rangi Tatu. Tatizo ni kwenye suala la dawa na vifaa hivyo, mimi najitahidi lakini narudishwa nyuma na watumisi wa afya wasio waadilifu ambao wanaiba dawa au kuzigawa kwa upendeleo kwa sababu ya rushwa,” alisema.
0 comments:
ASANTE KWA KUTEMBEA BLOGU YAKO::KARIBU SANA
Toa Mani yako Hapa usiogope Tuko PamojaPost a Comment