Monday, May 26, 2014

'Usife moyo mpendwa na mimi pia ni mkimbizi' ni maneno ya wakimbizi wa kisomali.


 Vijana wakimbizi wanaoishi katika kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani, nchini Kenya, Dadaab wamewatumia barua za kuwapa matumaini watoto wanaokumbwa na vita nchini Syria, ambao wamelazimika kutoroka vita na kukimbilia nchi jirani.

Wakimbizi hao wanaishi Dadaab Kaskazini mwa Kenya. Ni makao kwa wakimbizi 400,000 wengi wao waliotoroka vita, njaa na ukame nchini Somalia.
Shirika la misaada la kimataifa la Care International, ambalo hutoa misaada kwa wakimbizi hao, liliandaa mpango wa kuandikiana barua kati ya watoto hao na wale wa Syria wanaoishi katika kambi ya wakimbizi ya Amman nchini Jordan.

Barua zao ni za ujumbe wa matumaini , kuwapa moyo na ushauri wenzao wanaoishi katika mazingira sawa na wao. Wanawaita dada na ndugu zao.

Wengi wanawaasa kuhusu muhimu wa kusoma na kupata elimu wakiwa kambini.

''Mimi ni mkimbizi tu kama wewe''

Hibo Mahamed Dubow

''Nina uhakika kuwa ukisoma na kujitahidi maishani , utafanikiwa,'' ndio ujumbe wake Hibo Mahamed Dubow. "Cha mwisho ninakushauri kuwa usipoteze matumaini kwa sababu umekuwa mkimbizi kwa miaka mitatu pekee. Nini maoni yako kuhusu watu ambao wamekuwa wakimbizi kwa miaka 20?''

Ujumbe wake Hibo

''Kuweni mashujaa na marais wa sasa''

Dahir Mohamed aliandika barua ya matumaini

"Wapendwa dada zetu na kaka zetu, someni kwa bidii shuleni na muwe marais wapya wa Syria,'' alisema Dahir Mohamed.

Ujumbe wake Dahir Mohammed

''Tunahisi kama nyinyi tu''

Abshir Hussein aliandika ujumbe wa matumaini kwa wakimbizi wenzake

"Tunawaombea Mungu awape maisha mema na kwa msaada wake mtaweza kupata amani katika nchi yenu kwa sababu tunahisi tu kama nyinyi,'' ndivyo aliandika Abshir Hussein.
Watoto wa Syria nao pia walijibu.

Watoto wa Syria walipokea barua zao na picha. Picha hii ni ya Zakariye Mohamed akipokea barua yake pamoja na picha


Barua hizo zilipokewa vyema kwa mujibu wa shirika la Care International, na sasa wanaandika majibu yao kuwatumia watoto wa kambi ya Dadaab.
Share this article

0 comments:

ASANTE KWA KUTEMBEA BLOGU YAKO::KARIBU SANA

Toa Mani yako Hapa usiogope Tuko Pamoja

Post a Comment

 
Copyright © 2014 Chopa News • All Rights Reserved.
| Template Design by Anga Zio Team • Powered by Blogger online