Tuesday, July 22, 2014

UKAWA MSIZIBE MASIKIO; SAUTI ZINAWALILIA.

Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe.
 NIANZE safu hii kwa kumshukuru Mungu kwa kutulinda mmoja mmoja na hata taifa letu. Hakika yeye ni mwema. Nikumbushe tu kwamba viongozi wengi wa kisiasa, baadhi ya wananchi, taasisi za kiraia na madhehebu ya dini wanapaza sauti  kuwasihi Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) warejee bungeni.

Ni wito wa kila mpenda amani kuwataka wajumbe wa kundi hilo kuitikia ombi hilo na kuwaomba waache kuziba masikio kwani sauti ya wengi ni Baraka kwa Mungu.

Makundi hayo kwa nyakati tofauti, yamewataka wabunge kutoka Ukawa kutengua misimamo yao na kurejea bungeni ili kushindana kwa hoja na kukosoana wakiwa ndani ya Bunge la Katiba chini ya Mwenyekiti wao Samwel Sitta.

Hata hivyo, Ukawa wameeleza kuwa wamelisusa Bunge la Katiba, baada ya kujitokeza matusi, kejeli na maneno ya ubaguzi kutoka kwa wajumbe wa bunge hilo kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao wanadaiwa kuwa waliacha kujadili hoja za msingi na kuanza malumbano kinyume na dhamira ya kuundwa Bunge Maalum la Katiba.

Pia wanaeleza na kutoa masharti kuwa Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ijadiliwe kama ilivyo, isipunguzwe kipengele wala kifungu chochote na kwamba ushauri au maoni ya tume yabaki vilevile kama yalivyo na yasichakachuliwe.

Lakini naamini Ukawa wanasahau kwamba kazi ya Bunge Maalum la Katiba si kuipitia rasimu tu, bali pia ni kuijadili, kuongeza au kupunguza yaliyomo kwa masilahi ya taifa pale inapobidi. Nasisitiza bunge hilo lisiwe muhuri wa kuidhinisha kilichoandikwa na tume ya Jaji Warioba bali liwe huru kujadili na kufanya uamuzi.

Pia Ukawa wanamtupia lawama Rais Kikwete na kumtaja kuwa ndiye chimbuko la kuvurugika kwa mchakato huo baada ya kutoa maoni yake kama mkuu wa nchi, kwa maoni yangu hili dai limekosa nguvu ya hoja kwa kuwa JK ana haki ya kutoa maoni yake na yanaweza kupingwa au kukubaliwa ndani ya bunge wakati wa mjadala.

Kama alivyosimama Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba kwa kutetea msimamo wao, rais pia ana haki na wajibu wa kusimamia lile analoliamini kwa niaba ya serikali yake, sasa kazi ingekuwa kwa wabunge kuchambua na kuona hoja ipi inafaa na kamwe wabunge wa bunge hilo wasiwe bendera fuata upepo.

Tukumbushane tu kwamba madai ya kutaka Katiba Mpya yamekuwa yakidaiwa na kambi ya upinzani na baadhi ya wadau tangu mwaka 1992 tulipoanzisha vyama vingi vya siasa kwa kuelezwa kuwa Katiba ya mwaka 1977 haikidhi haja, imepitwa na wakati, ina upungufu wa msingi na si ya kidemokrasia pia inaruhusu mianya ya rushwa.

Wito ninaotoa ni kwamba pande zote ndani ya Bunge la Katiba zinatakiwa kuacha mizaha na mipasho, zijadili hoja, wanachokikataa au kukiafiki waonyeshe kama ni kweli hawakitaki kwa sababu zipi na kuafiki kwa minajili gani badala ya kuweka mbele itikadi au sera za vyama vyao.

Tulishuhudia  kundi la upinzani likiambiwa bungeni kuwa  ni wasaliti wa Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar, wakaitwa vibaraka na mawakala wa utawala ulioangushwa mwaka 1964 huku wengine wakiambiwa Zanzibar si kwao na hata rangi zao hazifanani na Afrika. Haya yalikuwa maneno mabaya kabisa tena ya kibaguzi.

Lakini naye Profesa Ibrahim Lipumba aliliita Bunge hilo ni la Interahamwe! Neno baya sana kutamkwa na kiongozi anayeaminika katika jamii tena msomi na mweledi kitaaluma katika uchumi kama yeye. Haya yote hayakustahili kutamkwa ndani ya Bunge la Katiba.

Madhali viongozi wa juu wakiwamo wanasiasa na viongozi wa madhehebu ya dini wanapiga kelele kuwataka Ukawa warejee bungeni, nafikiri ni wakati wao kukaa na kutafakari ushauri uliotolewa ili warejee bungeni, tukapiganie katiba mpya safi ya kulisukuma mbele taifa letu.

Ninaomba kikao cha Julai 24, mwaka huu ambacho amekiitisha Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samwel Sitta kifanyike kwa amani na maridhiano yapatikane.

Rasimu ya Katiba imesheheni mambo mengi muhimu, yanayohitajika kwa wakati tulionao. Ikiwa itakosekana kupatikana mwakani, anaweza akatokea rais mkorofi, asiyeambilika wala kushaurika akasema hana mpango wa kuunda katiba mpya na kuiona iliyopo inafaa na kukidhi haja, madai yataanza upya wakati nafasi tumeipata na tunaichezea.

Ikiwa hilo litatokea, kundi la Ukawa halitaachwa kubebeshwa lawama, nashauri Rasimu ya Katiba iwe ndiyo msingi wa mjadala katika bunge hilo ili kunusuru mchakato huo na baadaye Tanzania tupate katiba iliyo bora.
 Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Bonyeza Like hapo juu uwe wa kwanza kupata habari mpya. 

CHANZO:GPL

Share this article

0 comments:

ASANTE KWA KUTEMBEA BLOGU YAKO::KARIBU SANA

Toa Mani yako Hapa usiogope Tuko Pamoja

Post a Comment

 
Copyright © 2014 Chopa News • All Rights Reserved.
| Template Design by Anga Zio Team • Powered by Blogger online
back to top