Friday, April 4, 2014

Emmanuel Okwi ayeyuka Yanga na haijulikani kaelekea wapi.


Mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi.

SAKATA la mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi kudaiwa kususia mazoezi, sasa limeendelea mbele zaidi ya ilivyoelezwa awali.

Habari mpya ni kuwa Okwi, raia wa Uganda, amegoma kabisa hata kujiunga na wenzake walioweka kambi Bagamoyo na siyo kususia mazoezi pekee, kisa kikiwa ni kutaka kumaliziwa fedha zake za usajili ambazo inadaiwa bado anadai.

Kutokana na Okwi kugoma na kutoonekana kambini, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm alijikuta akianza kumsaka mchezaji huyo kwenye vyumba vya wachezaji jana asubuhi baada ya kuambiwa hajafika kambini.

Baada ya kuzunguka kila chumba bila mafanikio, Pluijm akaanza kuwauliza wachezaji kadhaa juu ya Okwi lakini wote wakasema hawajui alipo, ndipo akaamua kumfuata rafiki wa karibu wa mchezaji huyo, Hamis Kiiza ambaye naye ni raia wa Uganda.

Alipofika kwa Kiiza naye akampa jibu kama alilopewa na wachezaji wengine: “Sijui Okwi alipo.”

“Kocha anahangaika sana kumtafuta Okwi na hajui yupo wapi kwani leo asubuhi (jana) aliamka na kuanza kuwauliza wachezaji na baada ya kukosa jibu la kuridhisha, alimfuata Kiiza lakini nako aliambulia patupu,” alisema mtoa habari wetu.

Alipoulizwa mtu mwingine wa ndani ambaye naye yupo kambini juu ya suala hilo, alisema: “Okwi alimwambia…(anataja jina) kuwa bado kuna malipo yake ya usajili hawajamkamilishia, ndiyo maana ameamua kugoma kuja kambini kabisa.”

Inaelezwa kuwa Okwi bado anadai dola 40,000 (Sh milioni 64) ambazo zilisalia katika makubaliano ya awali wakati anatua klabuni hapo mwishoni mwa mwaka jana akitokea SC Villa ya Uganda.

Gazeti hili lilipomuuliza Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto juu ya sakata hilo alisema hana taarifa zozote kutoka kwa msimamizi wa kambi hiyo.

Alipotafutwa Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh ambaye yupo kambini, alisema: “Sina uwezo wowote wa kulizungumzia suala hilo ila wenye mamlaka ni katibu mkuu na ofisa habari ambao ndiyo wasemaji wa klabu.

“Kama wamekwambia kuwa hawajui lolote juu ya jambo hilo basi watakuwa wamegoma kukupa ushirikiano kwani suala hilo linajulikana,” alisema Hafidh.
Okwi alipotafutwa hakupatikana kwa kuwa simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila kupokelewa na baadaye haikupatikana kabisa.
SOURCE:GPL
Share this article

0 comments:

ASANTE KWA KUTEMBEA BLOGU YAKO::KARIBU SANA

Toa Mani yako Hapa usiogope Tuko Pamoja

Post a Comment

 
Copyright © 2014 Chopa News • All Rights Reserved.
| Template Design by Anga Zio Team • Powered by Blogger online
back to top