Saturday, June 21, 2014

Huyu ndie Mdada aliyepewa za Moto Baada ya Kukiuka Amri ya polisi ya kutocheza Khanga Moko Dar.


MNENGUAJI wa Kundi la Kanga Moko, Zawia Hamis  ambaye usiku wa Jumatano iliyopita alipigwa risasi mbili mwilini  na mtu aliyedaiwa ni askari polisi, ameweka undani wa sakata hilo.


Mnenguaji wa Kundi la Kanga Moko, Zawia Hamis akionyesha sehemu alikopigwa risasi mbili mwilini na mtu aliyedaiwa ni askari polisi.

Akizungumza na gazeti hili juzi nyumbani kwake Mwananyamala jijini Dar, majeruhi huyo alisema tukio hilo lilijiri maeneo ya Mwananyamala- Kisiwani karibu na Ofisi za Chama cha Wananchi (Cuf) na kuongeza kuwa, kisa ni kubishana na askari huyo aliyetaka kuzimwa kwa matarumbeta kutoka kwenye kikundi chao kilichokuwa kikipita eneo hilo.

“Sisi tulikuwa tukipita na matarumbeta, askari wakatusimamisha na kutuamuru tuyazime kisha kutaka kutukamata watupeleke kituoni eti serikali imekataza.

“Tuliwaambia mbona ni mapema sana kwani ilikuwa saa kumi alasiri na Kova alisema ngoma za Kanga Moko, Kigodoro na nyingine zisipigwe usiku. Pia tuliwaambia tulichokuwa tukikifanya si ngoma hasa, ni matarumbeta tunapita kuwaalika watu kuwa leo kuna shughuli sehemu.

Mnenguaji wa Kundi la Kanga Moko, Zawia Hamis akiwa hoi kitandani baada ya kujeruhiwa na risasi.

“Baada ya majibu hayo ndipo askari mmoja hakutaka hata kuendelea na mazungumzo, alitoa bastola kiunoni na kunipiga risasi mbili, moja kiunoni, nyingine kwenye mbavu halafu akapiga tena hovyo hewani risasi zilizobaki. Kwa kweli nimeumia sana,” alisema Zawia.

Mnenguaji huyo alisema kutokana na hali yake kuwa mbaya alipelekwa Kituo cha Polisi cha Mwinjuma na kupewa Polisi Fomu No. 3 (PF3) kisha kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kinondoni, Mwananyamala kwa ajili ya matibabu ambapo  kwa mujibu wake alitolewa risasi mbili.  
Baada ya kuzungumza na majeruhi huyo, waandishi wetu walikwenda kwenye Kituo cha Polisi Mwinjuma ambako ndiko alikoripoti PF3.

Askari mmoja wa kituo hicho (jina lipo) alisema hawezi kusema lolote kuhusu tukio huku akiweka wazi kwamba, afande aliyempiga risasi mnenguaji huyo anajulikana hivyo mlalamikaji anaweza kwenda mbele ya sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Dar, Camillius Wambura hakupatikana kwa simu juzi kuzungumzia tukio hilo lakini gazeti hili linaendelea kufuatilia.

Ungependa stori kama hizi zisikupite na zikufikie wakati wowote? niko tayari kukutumia wakati wowote iwapo utajiunga na mimi kwa kubonyeza Like hapo juu

Share this article

0 comments:

ASANTE KWA KUTEMBEA BLOGU YAKO::KARIBU SANA

Toa Mani yako Hapa usiogope Tuko Pamoja

Post a Comment

 
Copyright © 2014 Chopa News • All Rights Reserved.
| Template Design by Anga Zio Team • Powered by Blogger online